Uganda: Dkt. Flavian Zeija ateuliwa Jaji Mkuu mpya

Dkt. Flavian Zeija aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Uganda na Mheshimiwa Rais Yoweri Museveni tarehe 22 Januari 2026, na akaapishwa rasmi tarehe 24 Januari 2026 mjini Kisozi.
Anamrithi Jaji Alfonse Owiny-Dollo, aliyestaafu tarehe 18 Januari 2026 baada ya kufikia umri wa kikatiba wa miaka sabini (70).
Kabla ya kuteuliwa kwake katika nafasi hii ya juu zaidi ya mahakama, Dkt. Zeija aliwahi kushika nyadhifa za Jaji Mkuu Msaidizi wa Mahakama Kuu (Principal Judge) na baadaye Naibu Jaji Mkuu (Deputy Chief Justice). Kwa uteuzi huu, anakuwa Jaji Mkuu wa kumi na mmoja (11) katika historia ya mahakama ya Uganda.
Kwa wadhifa wake kama Mkuu wa Mhimili wa Mahakama, Jaji Mkuu anaongoza Mahakama ya Juu ya Uganda (Supreme Court) na kusimamia kwa ujumla utawala na uendeshaji wa mahakama zote nchini.
Safari ya kitaaluma ya Dkt. Flavian Zeija inaonesha uzoefu wa kipekee unaojumuisha utendaji wa uwakili, taaluma ya ualimu wa vyuo vikuu, na utumishi wa juu wa kimahakama.
- Kazi ya Uwakili na Sekta Binafsi
Kabla ya kujiunga na mahakama, Dkt. Zeija alifanya kazi ya uwakili kwa zaidi ya miaka kumi na minane (18), akihudumu kama wakili na mshauri wa kisheria, hasa kwa benki na mashirika binafsi.
- Kazi ya Kitaaluma
Sambamba na kazi yake ya uwakili, Dkt. Zeija alijenga taaluma mashuhuri ya kitaaluma kama mhadhiri na mtafiti. Alihudumu kama Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Makerere, Chuo Kikuu cha Kikristo cha Uganda (UCU), na Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Makerere (MUBS).
Aidha, alikuwa Mkuu mwanzilishi wa Idara ya Sheria ya Biashara katika MUBS.
- Maendeleo ya Kazi ya Kimahakama
- 2016: Aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Uganda, akihudumu kama Jaji Mkazi wa Mkoa wa Mbarara;
- Desemba 2019: Aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu Msaidizi (Principal Judge), akiwa na jukumu la kusimamia Mahakama Kuu na mahakama za ngazi ya chini;
- Februari 2025: Alipandishwa cheo kuwa Naibu Jaji Mkuu (Deputy Chief Justice);
- Januari 2026: Aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Uganda, na hivyo kuwa wa 11 kushika nafasi hiyo.
Kwa kumbukumbu, uamuzi wa kuanzishwa kwa Mkutano wa Mamlaka za Mahakama za Kikatiba barani Afrika (CJCA) ulifikiwa katika Mkutano wa Umoja wa Afrika uliofanyika Kampala, Uganda, mwezi Julai 2010.
